Khalifa, Ambarak Ibrahim Salehe
(2013)
Usawiri wa masuala ya Kijinsia katika Lugha ya mashairi: Mifano kutoka Mashairi ya Bongo Fleva.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza masuala ya Kijinsia katika Lugha ya Mashairi: Mifano kutoka Mashairi ya Bongo fleva. Lengo hili limeweza kufanikiwa kutokana na kukamilika kwa madhumuni mahususi yaliyohusu, kubainisha tamathali za semi katika mashairi ya bongo fleva, kuonesha jinsi tamathali hizo zinavyosawiri mahusiano ya kijinsia, kubainisha nafasi ya mwanamke na mwanaume kama inavyosawiriwa na tamathali za usemi za mashairi ya bongo fleva na kuainisha tofauti baina ya wasanii wa kike na kiume katika kusawiri masuala ya kijinsia. Mapitio ya kazi tangulizi mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti yamepitiwa kwa kina kwa kuongozwa na nadharia za Simiotiki, Ufeministi na Umarx. Kwa upande wa uchambuaji, uchakataji na usanifishaji wa data, utafiti umetumia mbinu za ushiriki, usaili, hojaji na upitiaji wa nyaraka katika kukusanya data. Mbinu ya uchambuzi wa kimaelezo ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data za utafiti huu.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba, lugha ya mashairi ya bongo fleva inasawiri vilivyo masuala kijinsia ambapo wote mwanaume na mwanamke pamoja na sifa zao zinaelezwa katika mashairi hayo. Matokeo ya utafiti yanaendelea kuonesha kwamba, mwanamke anasawiriwa kama mama, mlezi, jasiri na shujaa, mshauri na mchapakazi katika jamii. Vile vile, anasawiriwa kama Malaya, mvivu wa kufikiri na kiumbe rahisi kudanganyika. Mwanaume kwa upande wake anasawiriwa kama kiongozi wa nyumba, kiumbe mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri, baba jasiri na shujaa. Vile vile, anasawiriwa kama mlevi, Malaya, mtelekeza watoto, kiumbe mwenye tama na asiyeridhika. Mwisho ni hitimishi, muhtasari na mapendekezo ya utafiti wa baadaye.
Actions (login required)
|
View Item |