Balele, Janeth Magubiki
(2025)
Kuchunguza Athari ya Maendeleo ya Sayansi aa Teknolojia katika Kipera cha Ngano za Jamii ya Wasukuma Wilayani Kahama.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu ulihusika na kuchunguza athari za maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kipera cha ngano za jamii ya Wasukuma wilayani Kahama. Utafiti ulikuwa na malengo mahsusi matatu ambayo ni: (1) Kubainisha ngano zitumikazo katika jamii ya Wasukuma wa Kahama mkoa wa Shinyanga; (2) Kubainisha umuhimu wa ngano katika jamii hiyo; na (3) Kubainisha athari ziletwazo na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ngano za jamii ya Wasukuma wa Kahama. Data za msingi za utafiti huu zilikusanywa kwa mbinu ya ushuhudiaji, mahojiano, na madodoso. Mjadala na uchambuzi wa data uliongozwa na nadharia ya naratorojia, huku programu za SPSS, na ATLAS.ti, zikitumika kuchambua data za madodoso. Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa ngano ni sehemu muhimu ya urithi wa utamaduni wa jamii ya Wasukuma, hususan wa eneo la Kahama. Watafitiwa walionesha kuwa na uelewa mkubwa juu ya dhana ya ngano, ambapo walizitafsiri kama visakale au visasili vinavyowasilisha maadili, historia na utambulisho wa kiutamaduni. Pia, ngano hutumika kutoa mafunzo, kuonya, na kuburudisha, huku zikisaidia kuimarisha mshikamano wa kijamii na urithishaji wa maarifa kati ya vizazi. Aidha, matokeo yalibainisha makundi mbalimbali ya ngano yaliyotumika katika nyakati tofauti kama vile wakati wa kazi maalum, mavuno, masika, sherehe za harusi, na kumbukizi za mashujaa, ambapo ngano hizo zilitumika kama nyenzo muhimu za kufundishia mila, desturi na maadili ya jamii. Vilevile, Wasukuma walisisitiza umuhimu wa ngano katika kudumisha mshikamano wa kijamii na kuhifadhi lugha ya Kisukuma kupitia simulizi za kijadi. Hata hivyo, maendeleo ya sayansi na teknolojia yameathiri usimulizi wa ngano za kiasili, kwani teknolojia imewezesha kuhifadhi simulizi hizo kupitia majukwaa ya kidijitali na kusababisha kupungua kwa usimulizi wa moja kwa moja wa kijadi. Utafiti huu unahitimisha kuwa ngano ni urithi muhimu wa Wasukuma unaodumisha maadili, historia, na utambulisho wa kijamii, ingawa maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadili mbinu za usimulizi na uhifadhi wake. Aidha, huu utafiti unapendekeza jamii, taasisi za elimu, na wizara husika zihakikishe urithi huu unadumishwa kwa kufundisha na kuhifadhi ngano kupitia programu za elimu na teknolojia za kisasa bila kupoteza uhalisia wake wa kitamaduni.
Actions (login required)
 |
View Item |