Senyamanza, Christopher Alexander
(2015)
Tathmini ya Mabadiliko ya Rara Mintarafu Maendeleo
ya Jamii.
Masters thesis, The Open University Of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia mabadiliko ya rara yaliyojitokeza kama matokeo ya maendeleo ya jamii yaliyofikiwa. Rara, tendi, visasili na visakale vya kishairi ni tanzu za ghani-masimulizi. Aidha, rara imefafanuliwa kama tungo za kishairi zinazoimbwa kwa kuambatana na ala ya muziki. Nyimbo za rara huweza kusimulia
matukio ya kweli kama vile kutangazwa kwa uhuru, kesi za mauaji, na majanga ya kiasili. Wakati mwingine husimulia matukio ya kubuni na mtambaji wa rara sharti awe fundi wa kupiga ala ya muziki. Sanaa hii ilikuwepo tangu mwanadamu
alipoanza kuzalisha na kutumia sanaa katika maisha yake. Hali hii inatuaminisha kwamba sanaa hii imebadilika tangu wakati huo mpaka leo. Hii kutokana na kuwa kama mwanadamu amebadilika kutokana na mpito wa wakati, kubadilika kwa
mazingira, na maendeleo yaliyofikiwa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, ni dhahiri kwamba sanaa hii nayo imebadilika. Utafiti huu umethibitsha haya kwa kuchunguza mabadiliko yake kifani na kimaudhui. Kwa kutumia nadharia za ubadilikaji mpya, sosholojia na simiotiki utafiti umethibitisha mabadiliko ya rara tangu awamu ya kabla na wakati wa ukoloni, baada ya uhuru miaka ya 1960-1967, wakati wa ujamaa na kujitegemea miaka ya 1967-1988 na wakati wa mfumo wa soko huria miaka ya 1988-2010. Matokeo ya utafiti huu yanabainisha kwamba kila awamu ya maendeleo
yaliyofikiwa na jamii yalizalisha sanaa iliyokuwa tofauti kimaudhui na kifani. Hali hii imeonekana kusukumwa na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni iliyokuwa imefikiwa na jamii. Kwa kawaida maisha halisi ya wanajamii huwa sambamba na mifumo ya maendeleo iliyofikiwa na wanajamii. Rara ambayo huihudumia jamii katika uhalisia wa maisha, ililazimika kubadilisha mtazamo kulingana na mazingira halisi.
Actions (login required)
|
View Item |