Athumani, Mkumba Rashidi
(2015)
Athari za Kiisimu za Lugha ya Kiswahili katika Lugha ya Kiyao.
Masters thesis, The Open University Of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu umechunguza jinsi lugha ya Kiswahili inavyoiathiri kiisimu lugha ya Kiyao. Lugha hizi zinatumiwa na Wayao kwa muda mrefu. Wataalamu wengi wanakubaliana kuwa lugha zinapokutana huwa zinaathiriana. Kwa hivyo utafiti huu
umechunguza athari ya Kiswahili katika Kiyao. Eneo lililohusika katika utafiti huu ni wilaya ya Songea, Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma. Pia wilaya ya Masasi
katika mkoa wa Mtwara. Mbinu zilizotumiwa kuwapata watafitiwa wa utafiti huu ni mbinu ya makusudi na mbinu ya usampulishaji mpokezano. Mbinu ya makusudi ilitumiwa ili kuwapata watafitiwa wanaoimudu vyema lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiyao ili kupata matokeo faafu. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Makutano ya Lugha na Nadharia ya Fonolojia ya Konsonanti Vokali. Nadharia ya Makutano ya
Lugha ilitumiwa kuonesha kukutana kwa lugha hizi mbili kunakozua athari za Kiisimu. Nadharia ya Konsonanti Vokali ilitumiwa kubaini namna Kiswahili kinavyoiathiri Kiyao sawia na michakato ya kiisimu katika ngazi ya silabi zilizounda maneno husika. Utafiti huu una sura tano: Sura ya kwanza imezungumzia vipengele vya utangulizi wa utafiti kama usuli, tamko la utafiti, malengo, sababu na upeo na
mipaka ya utafiti huu. Sura ya pili ni ya mapitio ya kazi tangulizi na nadharia za utafiti huu. Sura ya tatu imefafanua mbinu za utafiti huu.Sura ya nne imechanganua
data za utafiti huu na sura ya tano imetoa muhtasari, matokeo, mapendekezo na changamoto za utafiti huu. Utafiti huu umebaini kuwa Kiswahili kinaiathiri Kiyao na kwamba kuna michakato ya kifonolojia na kimofolojia inayojitokeza wakati wa kuathiriwa kwa lugha hii. Utafiti huu utatoa chachu kwa watafiti wengine kuendeleza tafiti zinazohusu maathiriano ya kiisimu miongoni mwa lugha za kiafrika.
Actions (login required)
|
View Item |