Almabrok, Mohamed Ibrahim
(2004)
Nomino za Kiarabu katika Ngeli za Kiswahili.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Tasnifu hii ni utafiti unaohusu Nomino za Kiarabu Katika Ngeli za Kiswahili.. Nadharia iliyotumika katika kazi hii kuhusu uwasilishaji na uchanganuzi wa data ni ile inayohusu maumbo ya maneno katika lugha; yaani nadharia yakimofolojia. Tasnifu nzima imeundwa na sura sitae
Sura ya kwanza inahusu utangulizi wa kazi nzima. Katika utangulizi, usuli wa tatizo umewekwa bayana. Dhana ya mwingiliano wa lugha imejadiliwa kwa kuhusishwa na kuingiliana kwa Kiswahili na Kiarabu, na matokeo ya kiisimu ya mwingiliano huo. Aidha dhana za mabadiliko ya lugha na
uazimaji wa kileksika zimefafanuliwa kwa kuzingatia lugha hizi mbili. Pamoja na usuli wa tatizo, sura hii pia imeonesha wazrwazi malengo ya utafiti huu, umuhimu wa utafiti, nadharia tete, maswali ya utafiti, matatizo yaliyojitokeza katika utafiti huu na mipaka ya utafiti mzima. Sura ya pili imeshughulikia mapitio mbalimbali ya maandishi yanayohusu nomina za Kiswahili na Kiarabu. Katika sura hii maana na uainishaji wa nomino za Kiswahili na Kiarabu vimeelezwakwa makini. Aidha ngeli za nomino na uchanganuzi wake katika Kiswahili umewekwa bayana; ijapokuwa katika Kiarabu mfumo wa ngeli hauko wazi ama haupo kabisa kama ilivyokatika lugha ya Kiswahili.
Sura ya tatu inahusu nadharia na mbinu zilizotumika katika utafiti huu. Katika sehemu hii, nadharia ya kimofolojia kwa
kuzingatia uwazi na mapungufu vimeelezwa wazi. Aidha eneo la
utafiti, wahusika-lengwa, namna ya ukusanyaji wa data,
muundo wa ukusanyaji wa data, mpango wa uchanganuzi wa data na zana zilizotumika katika utafiti, vyote hivyo vimefafanuliwa wazi. Kuhusu zana zilizotumika, utafiti huu umetumia uchunguzi wa maktaba, masaili na maswali ya dodoso.
Sura ya nne imehusika na mambo makuu mawili; uwasilishaji
na uchanganuaji wa data. Kwa kuwa nomino za Kiswahili zenye
asili ya Kiarabu (data) zilizokusanywa ni takribani elfu moja mia tano, uwasilishaji na uchanganuzi wa data umetumia robo ya data hizo, na orodha nzima ya data hizo imeambatishwa nyuma ya tasnifu hii kama kiambatisho A na E. Katika uwasilishaji na uchanganuzi, sura hii imeonesha nomino za Kiswahili zenye asili ya Kiarabu, nomino asilia za Kiarabu na matumizi ya nomino hizo katika lugha zote mbili. Uwasilishaji na uchanganuzi wa nomino zote zenye asili ya Kiarabu umezingatia sifa za kifonolojia, kimofolojia na kisemantiki. Aidha mpangilio wa nomino za Kiswahili zenye asili ya Kiarabu katika mfumo wa ngeli za Kiswahiliumepewa nafasi inayostahili. Sura ya tano imejadili nadharia ya ukopaji wa kiisimu. Nadharia
hii imefafanuliwa kwa kuzingatia nadharia-saidizi mbili za
Uchanganuzi-linganishi na ile ya Kisaikolojia ya Mwingiliano wa Lugha. Katika ufafanuzi zaidi, ulinganishaji na ulinganuaji wa nadharia hizi umeoneshwa wazi kwa kuzingatia mchango wa nadharia hizi na mada yetu ya utafiti. Aidha, mjadala wa nadharia hizi umefanywa kwa kuzingatia maswali ya utafiti kama yamepata majibu muafaka; na kama malengo ya utafiti yamefikiwa. Na hatimaye, muhtasari wa utafiti, mahitimisho yake na mapendekezo kadhaa kwa ajili ya utafiti zaidi vimetolewa katika sura ya sita na ya mwisho.
Actions (login required)
|
View Item |