Maendeleo ya lugha ya Kiswahili na Athari zake kwa Jamii ya Kiaarabu: Mtazamo wa Kilughawiya Jamii

Ababaker, Emad Ahmed (2013) Maendeleo ya lugha ya Kiswahili na Athari zake kwa Jamii ya Kiaarabu: Mtazamo wa Kilughawiya Jamii. ["eprint_fieldopt_thesis_type_phd" not defined] thesis, The Open University of Tanzania.

[thumbnail of Maendeleo_ya_Kiswahili_na_athari_zake_kwa_jamii_ya_Kiarabu_(1).pdf]
Preview
PDF
Download (270kB) | Preview

Abstract

Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza chimbuko na maendeleo ya Kiswahili na athari zake kwa jamii ya Kiarabu kupitia mtazamo wa Kilughawiya jamii. Lengo hili limeweza kufanikiwa kutokana na kukamilika kwa malengo mahususi yaliyohusu; kuchunguza chumbuko la lugha ya Kiswahili na sababu za madai kwamba Kiswahili kimeathiriwa sana na Kiarabu, kubainisha namna Kiswahili kilivyoiathiri jamii ya Kiarabu katika maisha yake ya kila siku na kufafanua maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika karne ya ishirini na moja na changamoto zake. Mapitio ya kazi tangulizi mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti yamepitiwa kwa kina kwa kuongozwa na nadharia ya Lugha kama Muundo Jamii, Kiswahili ni Kiarabu na Kiswahili ni lugha ya Vizalia yameshadidia kukomaa kwa kazi husika. kwa upande wa uchambuaji, uchakataji na usanifishaji wa data, utafiti umetumia mbinu za ushiriki, usaili, hojaji na upitiaji wa nyaraka katika kukusanya data. Mbinu ya uchambuzi wa kimaelezo ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data za utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa chimbuko la Kiswahili ni katika mwambao wa Afrika ya Mashariki. Hata hivyo zipo sababu mbalimbali zinazotumiwa na wale wanaodai kwamba Kiswahili kimeathiriwa sana na Kiarabu na hivyo kutoa hitimishi kwamba Kiswahili asili yake ni Kiarabu. Sababu hizo ni pamoja Kiswahili kujengwa na msamiati mwingi wa lugha ya Kiarabu, Kiswahili kuwa na msamiati wenye lafudhi ya Kiarabu na ushairi wa Kiswahili asili yake ni dini ya Kiislamu na fasihi ya Kiarabu. Hata hivyo, matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba sababu hizo hazina mashiko ya kitaalimu katika kushadidia kile zinachoeleza. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanataalimu waliotafiti na kutoa madai hayo walikuwa ni wageni ambao hawakuwa na ujuzi wa kutosha kuhusiana lugha ya Kiswahili na utamaduni wake. Kwa matokeo haya Kiswahili kimeendelea kuonekana kuwa ni lugha yenye asili yake katika mwambao wa Pwani ya Afrika ya Mashariki na si Kiarabu wala lugha ya Vizalia. Kutokana na ukweli huo Kiswahili kimeendelea kuwa lugha ya matumizi mapana na kuiathiri jamii ya Kiarabu inayoishi mwambaoni mwa Pwani ya Afrika ya Mashariki katika maisha yake ya kila siku. Athari hizo zinaonekana katika masuala ya kidini, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi. Kutokana na Kiswahili kuwa ndiyo lugha ya matumizi mapana katika nchi mbalimbali za Afrika ya Mashariki kimeweza kuvuka mipaka na kutumika pia kimataifa. Kiswahili kimekuwa ni lugha inayotumika katika ngazi mbalimbali za kielimu, lugha ya kupashana habari kitaifa na kimataifa na lugha ya kuwasilishia fasihi ya kitaifa na kimataifa. Haya ndiyo maendeleo yaliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika karne hii ya ishirini na moja. Mwisho, tumetoa hitimisho kuu la utafiti ambalo kwalo tumeainisha maeneo mbalimbali ya kiutafiti yanayoweza kuibuliwa kuhusiana na lugha ya Kiswahili na masuala ya kinadharia kwa ujumla.

Item Type: Thesis (["eprint_fieldopt_thesis_type_phd" not defined])
Subjects: 400 Language > 490 Other languages
Divisions: Faculty of Arts and Social Sciences > Department of Linguistics and Literary Studies
Depositing User: Mr. Administrator OUT
Date Deposited: 18 Dec 2015 12:09
Last Modified: 02 Jan 2017 13:57
URI: http://repository.out.ac.tz/id/eprint/508

Actions (login required)

View Item View Item