Juma, Ali Khamis
(2024)
Dhamira za Nyimbo za Michezo ya Watoto Zinavyosaidia Kuwajenga Ujasiri na Tabia Njema katika Jamii ya Wazanzibari.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti ulilenga kuchunguza dhamira za nyimbo za michezo ya watoto zinavyosaidia kuwajenga ujasiri na tabia njema katika jamii ya Wazanzibari. Utafiti ulikuwa na malengo mahususi matatu; mosi, kubainisha nyimbo za michezo ya watoto, mantiki na miktadha ya uimbaji katika jamii ya Wazanzibari. Pili, kuchambua dhamira za nyimbo teule za michezo ya watoto katika jamii ya Wazanzibari. Na tatu, kuonesha jinsi dhamira za nyimbo hizo zinavyosaidia kuwajenga ujasiri na tabia njema.Mbinu za ushuhudiaji, usaili na majadiliano zilitumika katika ukusanyaji wa data ambapo data hizo zilichambuliwa kwa kutumia mkabala wa maelezo. Nadharia za Uchambuzi Matini na Mwitikio wa Msomaji zilitumika kuongoza uchambuzi na uwasilishaji wa data za utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwaUtafiti huu ulibainisha mantiki na miktadha ya uimbaji wa nyimbo za michezo ya watoto. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa kuna nyimbo mbalimbali za michezo ya watoto ambazo zina maana tofauti tofauti na huimbwa katika miktadha mbalimbali. Miongoni mwa nyimbo hizo ni Duara, Moja mbili tatu, Mpilipili, Panya, Maji ya moto, Nalia na A e i o u, Tuamkapo asubuhi, Kidabwada, Turukeruke, Unakwenda wapi, Ndege kumi porini na Watoto wazuri. Nyimbo nyingine ni Baba kasafiri, Kificho, Mnara wa baba, Kaskazi, Sukari ya Mahonda, Ndugu yetu na Twende sikukuu. Nyimbo hizo huimbwa katika miktadha ya shuleni, nyumbani na mitaani, wakati wa mchana, jioni na usiku wa mapema. Kuhusu dhamira za nyimbo, matokeo ya utafiti yanabainisha kwamba nyimbo za michezo zina dhamira mbalimbali kulingana na mahitaji ya jamii. Miongoni mwa dhamira hizo ni pamoja na kuwajenga watoto kiakili na kifikira, kuwafunda na kuwaendeleza katika maadili mema, kuwaburudisha na kuwastarehesha. Dhamira nyingine ni pamoja na kuwajengea watoto mioyo ya kizalendo, kutafuta elimu, kupanga malengo katika maisha, kuwafundisha kutamka maneno ya lugha, kuwafundisha kuhesabu na kuwajengea uwezo wa uvumbuzi. Pia, hulenga kuwasaidia watoto katika kuwakuza kimwili na kimaadili kulingana na jamii wanayoishi. Kuhusu jinsi nyimbo za michezo ya watoto zinavyosaidia kuwajenga ujasiri na tabia njema, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa michezo ya watoto inawajenga ujasiri kwa huwakuza kiakili na kifikra, kufanyakazi kwa bidii, kuepuka utegemezi katika maisha, kutafuta elimu na kupanga malengo katika maisha yao ya kila siku. Kuhusu tabia njema, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa michezo huwakuza watoto kuwa na maadili mema, kuwa na moyo wa kizalendo, kuepuka kiburi, kufanya mazoezi ya viungo na kuwapenda wazazi. Kwa hakika dhamira hizo, huwajenga watoto kuwa na tabia njema katika jamii ambapo hufanya mambo yanayokubalika na kuacha mambo yote yasiyokubalika katika jamii yao. Mtafiti anapendekeza kwa wazazi na serikali kutilia maanani umuhimu wa nyimbo na michezo ya watoto kwa kujumuishwa katika mitaala ya elimu. Mwisho, mtafiti anapendekeza tafiti zaidi zifanyike kuchunguza umuhimu wa michezo ya watoto kwa jamii ya baadaye.
Actions (login required)
 |
View Item |