Lenjima, Jemima
(2024)
Uchunguzi wa Maumbo, Maana na Vigezo vya Utoaji Majina ya Asili ya Watu Katika Jamiilugha ya Wagogo.
Doctoral thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu umechunguza maumbo, maana na vigezo vya utoaji wa majina ya asili ya watu katika jamiilugha ya Wagogo. Utafiti uliofanyika ulikuwa na malengo mahususi matatu ambayo ni kuainisha majina ya asili ya watu, kuchanganua maumbo na maana za majina ya asili ya watu na kubainisha vigezo vya utoaji majina ya asili. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili ambazo ni nadharia ya Uumbaji ya Sapir, (1958) na nadharia ya Mofolojia Leksika kwa mujibu wa Kiparsky, (1982). Data za utafiti zilikusanywa katika mkoa wa Dodoma, wilaya za Mpwapwa na Chamwino, katika vijiji vinne. Vijiji hivyo ni Mima na Gulwe kutoka katika wilaya ya Mpwapwa pamoja na vijiji vya Mvumi Misheni na Handali kutoka katika wilaya ya Chamwino vilipitiwa na mtafiti. Jumla ya watoa taarifa arobaini na nane (48) walihusika kutoa taarifa zilizohusiana na mada ya utafiti. Watoa taarifa hao waliteuliwa kwa kutumia usampulishaji usonasibu. Data za utafiti zilikusanywa uwandani kwa kutumia mbinu ya mahojiano na majadiliano ya kundi lengwa. Utafiti ulitumia mkabala wa kimaelezo, majedwali na baadhi ya data zilichanganuliwa kwa kutumia michorati. Matokeo ya utafiti yamedhihirisha aina kumi na sita (16) za makundi ya majina na jumla ya majina mia nne sitini na tatu (463) yaliyokusanywa. Utafiti ulibaini kuwepo kwa makundi kumi na tatu (13) ya maumbo kwa kuzingatia aina ya jina husika na namna vijenzi vya jina hilo vilivyopangwa kupitia ngazi Leksia. Vile vile utafiti umeweza kubaini maana za baadhi ya maumbo yaliyounda nomino husika. Maumbo yaliyopatikana yamechanganuliwa kwa kutumia kanuni kumi na tatu (13). Utafiti pia umedhihirisha uwepo wa vigezo kumi na tatu (13) vinavyotumika katika utoaji majina ya asili ya watu kwa jamiilugha ya Wagogo kama lengo mahususi la tatu lilivyobainishwa. Aidha, utafiti huu umependekeza kwa tafiti nyingine kufanyika katika kuchunguza maumbo ya majina kwa kuangalia jinsi mofu zinavyoweza kuathiriana kisemantiki na kisintaskia katika jamiilugha ya Wagogo kwani tafiti hizo zitasaidia watafiti wengine kuifahamu lugha ya Kigogo.
Actions (login required)
 |
View Item |