Makosa ya Kisarufi katika Vyombo vya Habari vya Tanzania: Uchunguzi wa TBC1, ITV na STAR TV.

Mushumbwa, Alcheraus Rwegasila (2022) Makosa ya Kisarufi katika Vyombo vya Habari vya Tanzania: Uchunguzi wa TBC1, ITV na STAR TV. Masters thesis, The Open University of Tanzania.

[thumbnail of ALCHERAUS RWEGASILA MUSHUMBWA.pdf] PDF - Submitted Version
Download (1MB)

Abstract

Utafiti huu ulichunguza makosa ya kisarufi kwenye vyombo vya habari vya Tanzania. Umakini uliwekwa kwenye chaneli za TBC1, ITV na STAR TV. Utafiti uliongozwa na malengo matatu: Kuchunguza aina za makosa ya kisarufi katika vyombo vya habari; sababu za kufanyika kwa makosa ya kisarufi; na, hatua za utatuzi wa makosa hayo. Ili kutimiza malengo hayo, data zilikusanywa kutoka uwandani na maktabani kwa kutumia mbinu za usomaji wa matini, usikilizaji na utazamaji wa taarifa za habari, na hojaji. Aidha, nadharia mbili ziliongoza ukusanyaji na uchambuzi wa data za utafiti huu. Nadharia hizo ni Uchanganuzi wa Habari Kisarufi ya van Dijk (1988) na nadharia ya Uchanganuzi Makosa ya Corder (1976). Mkabala wa kitaamuli ulitumika katika kuchambua data na kuwasilisha matokeo ya utafiti. Data zilichanganuliwa na kufafanuliwa kwa maelezo na mifano ya kutosha. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kuna makosa mbalimbali ya kisarufi katika vyombo vya habari vya Tanzania kama makosa ya kimsamiati, kimatamshi, kimaumbo, kimuundo na kisemantiki. Pia, utafiti ulibaini kuwa kuna sababu za kufanya makosa ya kisarufi kwenye vyombo vya habari ambazo ni kukosa umahiri wa lugha (Kiswahili), athari ya lugha ya kwanza, kasumba, kutomudu sarufi ya Kiswahili, ufahamu wa lugha zaidi ya moja na ukosefu wa taaluma ya lugha kwa wanahabari. Vilevile, hatua za kuchukua ili kuepuka makosa zilizopendekezwa ni ufundishaji wa taaluma ya lugha kwa wanahabari, utoaji wa semina za matumizi sahihi ya lugha, vyombo vya habari kuajiri au kutumia wataalamu wa lugha, kutungwa kwa sheria za matumizi ya lugha na kufanya uhariri kwa kina kabla ya kutoa habari. Kutokana na utafiti huu, kuna haja ya tafiti nyingine kuendelea kufanyika kuhusu makosa mengine ya lugha yanayofanyika katika vyombo vya habari pamoja na athari zake. Maneno Makuu: Kimatamshi, Kimaumbo na Kisintakisia

Item Type: Thesis (Masters)
Subjects: 400 Language > 490 Other languages
Divisions: Faculty of Arts and Social Sciences > Department of Linguistics and Literary Studies
Depositing User: Mr Habibu Kazimzuri
Date Deposited: 05 May 2023 09:50
Last Modified: 05 May 2023 09:50
URI: http://repository.out.ac.tz/id/eprint/3621

Actions (login required)

View Item View Item