Butoyi, Dieudonné
(2022)
Tathmini ya Makosa ya Kisarufi ya Wanafunzi wa Kingwana Wanaojifunza Kiswahili Sanifu: Uchunguzi Kifani wa Vyuo Vikuu vya Burundi.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu ulilenga kutathmini makosa ya kisarufi ya wanafunzi wanaoongea Kingwana kama L1 wanaojifunza Kiswahili sanifu kama lugha ya kigeni. Malengo mahususi yaliyoongoza utafiti huu yalikuwa kubaini aina za makosa ya kisarufi yanayofanywa na wanafunzi wa lahaja ya Kingwana wanaojifunza Kiswahili sanifu, kutathmini viwango vya ujitokezaji wa aina mbalimbali vya makosa hayo na kuchunguza sababu za makosa ya kisarufi katika Kiswahili Sanifu. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uchanganuzi makosa (UM) iliyoasisiswa na Stephen Pit Corder (1967). Utafiti huu ulifanyika kwenye vyuo vikuu vitano na wanafunzi mia moja walishiriki.Mbinu za kukusanyia data zilikuwa mapitio ya nyaraka, ushuhudiaji na hojaji. Uchanganuzi wa data ulidhihirisha makosa ya kifonolojia yaliyojitokeza kwa kiasi cha 41.76%, makosa ya kimofolojia kwa kiasi cha 24.48% na makosa ya kisintaksia na kimofosintaksia kwa kiasi cha 33.75%. Uhamishaji wa mifumo ya Kingwana kwenda Kiswahili sanifu, kutojua kanuni za sarufi ya Kiswahili sanifu, ufupishaji wa vipashio na matumizi ya kanuni fulani kupita kiasi ndivyo vilivyodhihirika kuwa sababu za makosa hayo. Uhamishaji ulisababisha makosa yanayolingana na 55.60% ambapo kutojua kanuni kulisababisha makosa 31.92%. Matumizi ya kanuni fulani kupita kiasi yalisababisha makosa 8.12% ilihali ufupishaji ulisababisha makosa 4.34% kwa jumla ya makosa yote 874. Kutokana na matokeo hayo, utafiti huu umependekeza kuwa walimu wa Kiswahili nchini Burundi waimarishe ufundishaji wa Kiswahili na wanafunzi wafanye juhudi kujifunza Kiswahili. Pia utafiti unaiomba serikali ya Burundi kuweka na kuboresha sera ambayo ingeyapa kipau mbele mafunzo ya lugha ya Kiswahili.Mwishoni, kumependekezwa tafiti zingine kama vile uchunguzi wa makosa ya kisemantiki na uchunguzi wa launi za lahaja ya Kingwana.
Actions (login required)
|
View Item |