Ally, Nasra Habibu
(2020)
Athari za Mofu Ambishi na Nyambulishi katika Uundaji wa Vitenzi vya
Kisambaa.
["eprint_fieldopt_thesis_type_phd" not defined] thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu umechunguza na kuchanganua kuathiriana kwa mofu ambishi na nyambulishi
katika uundaji wa vitenzi vya Kisambaa. Katika uchunguzi na uchanganuzi huo, utafiti huu
pia umedhihirisha mashartizuizi yanayotawala uambikaji wa mofu katika kitenzi cha
Kisambaa. Uchambuzi na uwasilishaji wa data, katika utafiti huu umefanywa kwa
kuongozwa na Nadharia ya Umbo Upeo iliyoasisiwa na Prince na Smolesky. Data za utafiti
huu zilikusanywa kutoka tarafa ya Mlalo Wilaya ya Lushoto, maeneo ambako Wasambaa
wanapatikana. Data hizo zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya usaili na usomaji wa
maandiko. Utafiti huu umebaini kuwa mofu ambishi na mofu nyambulishi zinapoambikwa
katika mzizi wa kitenzi cha lugha ya Kisambaa zinaathiriana. Kuathiriana huko
kumebainishwa kwa kuzingatia mashartizuizi yanayotawala mfuatano na mpangilio wa
mofu katika kitenzi cha Kisambaa. Mofu ambishi na nyambulishi ambazo huathiriana ni
pamoja na mofu ya mofimu ya njeo, ukanushi, masharti, kutendea, utendeshi, ufanyikaji
sana, kutendeka na mofu ya mofimu ya urejeshi. Mofu hizo huathiriana katika kudondoshwa
kwa mofu, kubadili nafasi ya utokeaji wa mofu na kubadilika kwa umbo la mofu
inayoathiriwa pale zinapokaa pamoja kuunda kitenzi chenye maumbo mbalimbali
yanayokubalika katika Kisambaa. Matokeo ya kuathiriana huko ni kupatikana kwa maumbo
mbalimbali ya vitenzi yenye fahiwa tofauti tofauti. Maumbo hayo ya vitenzi yenye
mabadiliko ni kama vitenzi vyenye ukanushi, masharti, vitenzi katika hali ya kutendwa,
kutendea, urejeshi na utendeshi. Aidha, utafiti huu unapendekeza kuwa tafiti nyingine katika
lugha ya Kisambaa kuhusu maumbo ya vitenzi na namna mofu zinavyoweza kuathiriana
kisemantiki na kisintaksia zinahitajika. Vilevile kuna haja ya kuzitafiti zaidi lahaja katika
lugha ya Kisambaa. Pamoja na hayo suala la toni katika lugha ya Kisambaa ni muhimu
litafitiwe kwa kina.
Actions (login required)
|
View Item |