Saro, Stanley Julius
(2017)
Kuchunguza Usawiri wa Mwanamke katika Riwaya: Mfano wa Riwaya ya Utengano.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Mada ya utafiti huu ni kuchunguza usawiri wa mwanamke katika riwaya kwa kurejelea riwaya ya Utengano. Mada hii imefungamana vizuri na lengo kuu la utafiti huu lililovunjwa katika malengo mahususi mawili. Malengo hayo ni kuchambua usawiri wa mwanamke katika riwaya ya Utengano na kubainisha uhalisia wa usawiri wa mwanamke katika riwaya ya Utengano kwa jamii ya leo. Ili kutimiza malengo haya mahususi ya utafiti wetu tulikusanya data kwa kutumia mbinu za usomaji makini na upitiaji wa nyaraka maktabani na kuzichambua kwa kutumia mkabala wa kimaelezo na nadharia ya Ufeministi.
Utafiti umebaini kuwa mwanamke anasawiriwa katika hali mbalimbali ndani ya riwaya teule ikiwa ni pamoja na mwanamke ni kiumbe tegemezi, mwanamke ni kiumbe mpenda starehe, mwanamke ni malaya, mwanamke ni kiumbe muovu na mwanamke ni kiumbe jasiri. Pia imebainika kuwa mwanamke anasawiriwa kama kiumbe mchapakazi, kiumbe wa ndani, kiumbe mtiifu na kiumbe wa kuteswa. Usawiri huu wa mwanamke katika riwaya ya Utengano unaonekana kuwa na uhalisia katika maisha ya leo ya jamii kwani bado mwanamke anaguswa na usawiri huu katika maisha yake ya kila siku.
Actions (login required)
|
View Item |