Bavuai, Asha Iddi
(2017)
Muundo wa Kirai Nomino katika lahaja ya Kimakunduchi.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu umechunguza muundo wa kirai nomino katika lahaja ya Kimakunduchi. Malengo ya utafiti yalikuwa ni kubainisha vipengele vya muundo wa kirai nomino katika lahaja ya Kimakunduchi; kuelezea utaratibu au mpangilio wa vipengele vya muundo wa kirai nomino na lengo la tatu; ni kujadili dhima za kisarufi za kirai nomino. Utafiti huu ulitumia mkabala wa kimaelezo katika kukusanya na kuchambua data, huku nadharia ya sarufi miundo virai na dhana yake maarufu ya eksibaa ikiongoza utafiti huu. Utafiti ulifanyika Makunduchi mkoa wa kusini Unguja na ulihusisha shehia tatu ambazo ni shehia ya Kiongoni, shehia ya Nganani na shehia ya Mzuri.Watafitiwa walikuwa ni wazungumzaji asilia wa lahaja ya Kimakunduchi. Watafitiwa hao walichaguliwa kwa kutumia usampulishaji kusudio ambao mtafiti anachagua sampuli kulingana na malengo maalumu. Data za utafiti zilikusanywa kwa kutumia njia ya hojaji na uchunguzi makini kupitia shughuli za kijamii kwa mfano mwaka kogwa, sherehe za harusi, maziko na kadhalika. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kutumia mkabala stahilifu ambao ni ule unaotumia maelezo kulingana na data zilizopatikana kutoka kwa watafitiwa. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya sarufi miundo virai na dhana yake maarufu ya eksibaa. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba muundo wa kirai nomino katika lahaja ya Kimakunduchi una sifa za kimuundo ambazo hazipo mbali na lahaja nyingine pamoja na Kiswahili sanifu. Vile vile muundo wa kirai nomino katika lahaja ya Kimakunduchi umeonekana kuwa sawa na ule wa lugha za Kibantu na lahaja za Kiswahili kama ilivyoonyeshwa na wataalamu tofauti.
Actions (login required)
|
View Item |