Abdallah, Zuhura Ali
(2019)
Kuchunguza Uhalisiajabu na Dhamira katika riwaya za Kusadikika na Adili
na Nduguze.
Masters thesis, The Open University of Tanzania.
Abstract
Utafiti huu unahusu Kuchunguza Uhalisiajabu na Dhamira katika riwaya za
Kusadikika na Adili na Nduguze. Lengo kuu ni “Kuchunguza Uhalisiajabu na
Dhamira katika Kusadikika na Adili na Nduguze.” Riwaya hizi ziliandikwa na
Shaaban Robert. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Uhalisiajabu kwa lengo la
kwanza na swali la kwanza la utafiti. Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji imetumika
kwa lengo la pili na swali la pili la utafiti huu. Mbinu iliyotumika kukusanyia data
ilikuwa ni mbinu ya Usomaji Makini mbapo mtafiti alizisoma kwa kina riwaya teule
huku akidondoa data ambazo hatimae zilijibu maswali ya utafiti huu. Data za utafiti
huu zilichambuliwa na kuwasilishwa kwa mkabala wa kimaelezo na kitakwimu. Kwa
ujumla utafiti huu uliongozwa na malengo mawili na maswali mawili ya utafiti.
Lengo la kwanza lilikuwa: Kubainisha vipengele vya uhalisiajabu katika riwaya ya
Kusadikika na Adili na Nduguze. Lengo hilo limekwenda sambamba na swali la
kwanza la utafiti lisemalo: Ni Vipengele vipi vya Uhalisiajabu vilivyobainishwa
katika riwaya ya Kusadikika na Adili na Nduguze?Matokeo ya utafiti huu
yameonesha kuwa riwaya teule zimetumia vipengele vya uhalisiajabu kama vile;
utatizaji wa wakati, masimulizi ya kihalisiajabu, usawiri wa wahusika wa
kihalisiajabu, motifu za safari za kihalisiajabu, mitindo ya uumbuzi na udenguzi, na
mandhari ya kihalisiajabu. Lengo la pili la utafiti huu lilikuwa: Kubainisha dhamira
za uhalisiajabu katika riwaya ya Kusadikika na Adili na Nduguze. Lengo hilo
limewiana na swali la pili la utafiti huu lisemalo: Ni dhamira zipi za uhalisiajabu
zilizobainishwa katika riwaya ya Kusadikika na Adili na Nduguze? Matokeo ya
utafiti huu yamedhihirisha dhamira mbalimbali za uhalisiajabu kama ifuatavyo:
Umuhimu wa sheria, uongozi mbaya, ukweli, ukombozi, umuhimu wa huduma za
kijamii, ulafi, wivu na choyo. Riwaya ya Adili na Nduguze imebainisha dhamira za:
Usaliti, migongano ya mifumo ya kiuchumi ulimwenguni, ukoloni, ukweli, uongozi
bora na utabaka.
Actions (login required)
|
View Item |